Qatar yampa hifadhi kamanda mwandamizi wa zamani wa al-Shabab
Aliyekuwa kamanda wa ngazi za juu wa kundi la kitakfiri la al-Shabab, Muhammed Said Atam amepewa hifadhi na serikali ya Qatar.
Kanali ya televisheni ya Universal TV ya Somalia imeripoti kuwa, Atam ambaye alitangaza kuliasi kundi hilo la kigaidi mwaka 2014 yuko Doha, baada ya utawala wa Qatar kumpa hifadhi. Imearifiwa kuwa, Atam alikuwa kamanda wa kikosi cha al-Shabab katika eneo la milima la Galgala, magharibi mwa mji wa Bossaso, makao makuu ya Puntland. Habari zinasema kuwa, Atam amepokewa Doha kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali za Doha na Mogadishu. Mwaka 2012, Muhammed Said Atam, alitangaza kuwa na mafungamano na kundi la al-Shabab, lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda. Miongoni mwa makamanda wengine waandamizi wa al-Shabab ambao waliliasi kundi hilo la kigaidi na kujisalimisha kwa serikali ya Somalia ni pamoja na Sheikh Hassan Dahir Aweys mwaka 2013 na Zakariya Ismael, ambaye alikuwa mkuu wa kitengo cha ujasusi wa magaidi hao, mwaka 2014. Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alitangaza msamaha kwa wanamgambo wa al-Shabab ambao watajisalimisha.