Watu kadhaa wauawa katika mripuko wa bomu Libya
Gari lililokuwa limetegwa bomu limeripuka katika mji wa Benghazi wa mashariki mwa Libya na kuua na kujeruhi watu kadhaa.
Takwimu za hivi karibuni za hospitali za Libya zinaonesha kuwa, wanajeshi wawili wa serikali wameuawa na wengine wanne kujeruhiwa baada ya kuripukiwa na bomu la kutegwa garini huko Benghazi, mashariki mwa Libya.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Libya, hadi hivi sasa hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusiana na shambulio hilo.
Katika miezi ya hivi karibuni mji wa Benghazi umekumbwa na miripuko mingi ambayo imesasabisha makumi ya watu kuuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa.
Askari wanaoliunga mkono bunge la Libya katika mji wa Tobruk wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar ndio wanaodhibiti maeneo mengi ya Benghazi.
Libya ilitumbukia kwenye machafuko tangu mwaka 2011 wakati wa kampeni za kumpindua Kanali Muammar Gaddafi zilizokwenda sambamba na uingiliaji wa kijeshi wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO ambalo liliangamiza vibaya miundombinu ya nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.
Nchi hiyo hivi sasa imegawika sehemu mbili za Magharibi na Mashariki zinazoongozwa na serikali tofauti. Kukosekana serikali kuu yenye nguvu nchini Libya kumepelekea kukosekana utulivu wa kisiasa na kiusalama kama ambavyo kumetoa mwanya kwa magenge ya kigaidi kujipenyeza nchini humo likiwemo genge la wakufurishaji la Daesh (ISIS).
Aidha Libya imegeuka kuwa kituo kikuu cha magendo ya wanadamu hasa wale wanaokimbilia barani Ulaya.