El Sisi atetea siasa zake za kupambana na magenge ya kigaidi
(last modified Wed, 01 Mar 2017 07:18:48 GMT )
Mar 01, 2017 07:18 UTC
  • Rais Abdul Fattah el Sisi wa Misri
    Rais Abdul Fattah el Sisi wa Misri

Rais Abdul Fattah el Sisi wa Misri ametetea stratijia na mikakati ya serikali yake katika kupambana na magenge ya kigaidi kwenye mkoa wa Sinai Kaskazini.

Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo na kumnukuu Abdul Fattah el Sisi akisema jana usiku kwamba mikakati ya serikali yake ya kupambana na makundi yenye silaha katika mkoa wa Sinai Kaskazini ni sahihi kwani lengo la makundi hayo ni kuzusha fujo na ukosefu wa utulivu katika jamii ya Misri.

Amesema, mashambulizi ya makundi yenye silaha yanafanyika kwa nia ya kuwagombanisha wananchi wa Misri na baadaye kuisingizia serikali na kujaribu kuonesha kuwa imeshindwa kuwalinda wananchi wakiwemo Wakristo.

Itakumbukwa kuwa makumi ya familia za Wakristo zimeukimbia mji wa al Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini nchini Misri baada ya watu wenye silaha kuua Wakristo 7 wa Kibti.

Miripuko ya mabomu na mauaji yameongezeka katika Rasi ya Sinai, kaskazini mwa Misri

 

Genge la kigaidi la Daesh yaani ISIS wiki iliyopita lilisambaza mkanda wa video na kuahidi kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya jamii ya Wakristo nchini Misri.

Mwezi Disemba mwaka jana pia, genge hilo lilitangaza kuhusika na shambulio la kigaidi katika kanisa moja la Wakristo wa Kibti mjini Cairo ambapo watu 29 waliuawa kwenye shambulio hilo.

Misri ilianza kukumbwa na machafuko na mashambulizi ya kigaidi mwaka 2013 baada ya jeshi la nchi hiyo kumpindua Muhammad Morsi, rais wa kwanza kuchagulia kidemokrasia katika historia ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Tags