Tuzo ya kifahari ya Mo Ibrahim yakosa mshindi tena
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25810-tuzo_ya_kifahari_ya_mo_ibrahim_yakosa_mshindi_tena
Kama ilivyokuwa mwaka juzi, tuzo ya kifahari ya Mo Ibrahim mwaka jana 2016 pia imekosa mshindi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 01, 2017 12:37 UTC
  • Tuzo ya kifahari ya Mo Ibrahim yakosa mshindi tena

Kama ilivyokuwa mwaka juzi, tuzo ya kifahari ya Mo Ibrahim mwaka jana 2016 pia imekosa mshindi.

Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Simamizi ya Tuzo hiyo amesema bodi ya kutathmini viongozi imeshindwa kumpata kiongozi anayefaa kushinda tuzo hiyo ambayo iliweka viwango vya juu tangu kuasisiwa kwake zaidi ya muongo mmoja uliopita, kwa shabaha ya kuimarisha demokrasia na mfumo wa uongozi barani Afrika.

Dakta Salim Ahmed Salim amesema: "Ingawaje tunatambua mchango unaotolewa na viongozi mbali mbali barani Afrika, lakini lengo letu ni kuwatunuku viongozi wenye haiba na ustahiki wa kutuzwa, na mwaka jana hatujaona kiongozi yeyote aliyefikia kiwango hicho."

Baadhi ya marais wa Afrika waliostaafu hivi karibuni ambao mmoja wao alitazamiwa kupatiwa tuzo hii ni pamoja na John Dramani Mahama wa Ghana aliyekubali kushindwa katika uchaguzi wa mwaka jana, Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia na Yahya Jammeh wa Gambia. Rais mstaafu wa Kenya, Mwai Kibaki, Jakaya Kikwete wa Tanzania na Goodluck Jonathan wa Nigeria walikosa kushinda tuzo hii mwaka juzi 2014.

John Dramani Mahama, rais mstaafu wa Ghana

Tuzo hiyo ambayo tangu kuasisiwa kwake mwaka 2006 imetunukiwa viongozi wanne pekee, huwalenga marais ambao walichaguliwa kwa misingi ya demokrasia na kuhudumu katika muhula ulioanishwa na katiba pasina kung'ang'ania madaraka wala kuongoza kwa mkono wa chuma. Rais mstaafu wa mwisho kutuzwa tuzo ya Mo Ibrahim ni Hifikepunye Pohamba wa Namibia (2014). Wengine ni Pedro Pires wa Cape Verde (2011), Festus Mogae wa Botswana (2008) na Joaquim Chissano wa Msumbiji (2007).

Mshindi wa tuzo hii hukabidhiwa dola milioni 5 pesa taslimu katika muda wa muongo mmoja hivi na kisha dola laki mbili kila mwaka katika kipindi cha uhai wake.