Serikali ya Niger yaendelea kumshikilia Amadou licha ya kukaribia uchaguzi
(last modified Mon, 07 Mar 2016 06:42:28 GMT )
Mar 07, 2016 06:42 UTC
  • Serikali ya Niger yaendelea kumshikilia Amadou licha ya kukaribia uchaguzi

Hama Amadou, hasimu wa Rais Mahamadou Issoufou wa Niger katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais nchini humo, bado anaendelea kushikiliwa na vyombo vya dola licha ya kukaribia uchaguzi huo.

Serikali ya Niamey imetangaza kuwa, Amadou hatopewa fursa ya kushiriki katika kampeni za uchaguzi na kwamba ataendelea kusalia korokoroni hadi siku ya uchaguzi. Duru ya pili ya uchaguzi wa rais nchini Niger, imepangwa kufanyika tarehe 20 mwezi huu. Hama Amadou alitiwa mbaroni katikati ya mwezi Novemba mwaka jana kwa tuhuma za kuhusika katika magendo ya watoto wadogo na hadi sasa anaendelea kushikiliwa katika jela ya mji wa Filingué ulio umbali wa kilometa 180, kaskazini mwa mji mkuu Niamey. Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, tuhuma anazohusishwa nazo ni za kisiasa na kwamba tangu awali serikali ya Rais Mahamadou Issoufou iliamua kumtia ndani ili kumzuia asiweze kushiriki katika uchaguzi wa mwaka huu. Katika uchaguzi uliopita, Rais Issoufou alipata asilimia 48,4 huku hasimu wake huyo akipata asilimia 17,7 ya kura zote zilizopigwa na hivyo kushika nafasi ya pili. Licha ya kwamba amekuwa jela kwa miezi kadhaa sasa, lakini anaonekana kumnyima usingizi rais huyo na hivyo kuamua kutompa ruhusa ya kushiriki katika kampeni za uchaguzi.

Tags