Niger yachelea athari za kijamii na kiuchumi za mashambulizi ya Boko Haram
Rais wa Niger amesema ana wasiwasi wa athari hasi za mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram kwa hali ya kijamii na kiuchumi ya nchi hiyo.
Akizungumza na ujumbe wa wawakilishi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Rais Mahamadou Issoufou wa Niger ametaka wakimbizi wasaidiwe misaada ya kibinadamu na kuungwa mkono kimataifa. Baada ya safari yao nchini Niger, wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa waliotumwa barani Afrika waliekekea Cameroon na Chad na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa kikosi cha kijeshi cha kieneo cha mataifa kadhaa cha kupambana na Boko Haram ambapo pande mbili hizo zilijadili pia hatua zilizochukuliwa katika kuendesha mapambano dhidi ya kundi hilo la kigaidi.
Kikosi hicho cha pamoja cha kijeshi cha kupambana na Boko Haram hadi sasa kimeuwa wanamgambo 828 na kuwatia mbaroni wengine 615 wa kundi hilo. Kundi la kigaidi la Boko Haram lilibeba silaha na kuanzisha hujuma zake mwaka 2009 kwa shabaha ya kuasisi utawala eti wa Khilafa huko kaskazini mwa Nigeria na kisha likaanza kueneza mashambulizi yake huko Niger, Chad, na kaskazini mwa Cameroon. Kundi hilo limeuwa karibu watu elfu 15 katika kipindi cha miaka saba iliyopita katika nchi za Nigeria, Cameroon, Niger na Chad na kuwafanya raia wengine zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi.