Mripuko mwingine waukumba mji mkuu wa Somalia, Mogadishu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26284-mripuko_mwingine_waukumba_mji_mkuu_wa_somalia_mogadishu
Vyombo mbalimbali vya habari ya ndani na nje ya Somalia vimeripoti habari ya kutokea mripuko wa bomu leo Jumapili katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 12, 2017 10:21 UTC
  • Mripuko mwingine waukumba mji mkuu wa Somalia, Mogadishu

Vyombo mbalimbali vya habari ya ndani na nje ya Somalia vimeripoti habari ya kutokea mripuko wa bomu leo Jumapili katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu.

Mtandao wa habari wa Garowe nao umeripoti habari hiyo na kusema kuwa, mpiga picha mmoja wa televisheni ya Universal ya Somalia anayejulikana kwa jina la Abdihamid Mohamed Karzay amejeruhiwa vibaya kwenye mripuko huo. 

Kepteni Mohamed Hussein, afisa wa jeshi la polisi la Somalia amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, Karzay amejeruhiwa vibaya wakati gari yake iliporipuliwa na kitu chenye miripuko  katika wilaya ya Hamarweyne mjini Mogadishu wakati alipokuwa anaelekea kazini.

Miripuko ya mabomu ni jambo la karibu kila siku nchini Somalia

 

Afisa huyo amesema, mpiga picha huyo wa TV amewahishwa haraka kwenye hospitali ya karibu na eneo hilo kwa ajili ya matibabu. Hadi tunapokea habari hii hakukuwa na kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulio hilo la bomu.

Mmoja wa wafanyakazi wa televisheni ya Universal amesema, Abdihamid Karzay amejeruhiwa vibaya begani, mgongoni na pajani baada ya kuripukiwa na bomu lilikuwa limetegwa ndani ya gari yake.

Muuzaji mmoja wa duka amesema, kwa uchache raia wawili wamejeruhiwa baada ya gari ya mwandishi huyo wa habari kuripuka karibu na Msikiti wa Marwas huko Hamarweyne, karibu na soko lenye watu wengi.

Askari usalama wa Somalia wamefika kwenye eneo la tukio, lakini hakuna mtu yeyote aliyetiwa mbaroni.