UN yaitaka jamii ya kimataifa kukabiliana na tatizo la njaa nchini Somalia
Kwa mara nyingine Umoja wa Mataifa umeitaka jamii ya kimataifa kukabiliana na tatizo la njaa lililoikumba Somalia.
Farhan Haq, Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, UN imeitaka jamii ya kimataifa kukusanya kiasi cha Dola milioni 800 kwa minajili ya kuzuia mgogoro wa njaa unaoendelea kushuhudiwa nchini Somalia mwaka huu. Kwa mujibu wa Farhan Haq, hadi sasa kumekusanywa asilimia 31 ya kiasi hicho kutoka nchi wafadhili.

Wakati huo huo, António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ameitaka dunia kuingia katika mapambano hayo dhidi ya njaa nchini Somalia. Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, jumla ya nusu ya raia wa Somalia ambao ni karibu watu milioni sita na laki mbili wanahitajia msaada wa haraka huku watoto laki tatu na elfu 63 wakikabiliwa na hali mbaya sana ya utapiamlo. Hii ni mara ya tatu kwa taifa la Somalia la Pembe ya Afrika kukumbwa na njaa kali katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.

Hivi karibuni pia Shirika la Msalaba Mwekundu lilionya kuwa, jamii ya kimataifa ina muda wa miezi mitatu hadi minne kuokosoa maisha ya mamilioni ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa katika nchi za Somalia na Yemen.
