Maafisa wa kulinda amani wa Rwanda kuanza kuwasili Sudan Kusini kesho
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26790-maafisa_wa_kulinda_amani_wa_rwanda_kuanza_kuwasili_sudan_kusini_kesho
Jeshi la Polisi la Rwanda limetuma suhula na zana za kivita mjini Juba, zitakazotumiwa na kikosi kipya cha maafisa wake wa kulinda amani nchini Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 24, 2017 02:56 UTC
  • Maafisa wa kulinda amani wa Rwanda kuanza kuwasili Sudan Kusini kesho

Jeshi la Polisi la Rwanda limetuma suhula na zana za kivita mjini Juba, zitakazotumiwa na kikosi kipya cha maafisa wake wa kulinda amani nchini Sudan Kusini.

William Kayitare, Naibu Kamishna wa Polisi wa Rwanda amesema nchi hiyo itatuma maafisa wa polisi zaidi kwenda kulinda amani nchini Sudan Kusini.

Amesema maafisa 160 wa Kikosi cha Polisi cha Formed Police Unit (FPU) wataanza kuwasili katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba kuanzia kesho Jumamosi, na wataungana na askari wenzao 240 na washauri wa polisi 29 wa Rwanda ambao kwa sasa wanafanya kazi chini ya mwavuli wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa UNMISS.

Askari wa UNMISS wakiwasaidia watu kuondoka eneo lenye mapigano

Kaimu Kamishna wa Polisi wa Rwanda amesema: "Vikosi vyetu tulivyovituma nje ya nchi vinafanya kazi kitaalamu, kwa nidhamu na kuonyesha moyo wa kujitolea na kujituma, na ndipo vimekuwa vikiaminiwa na Umoja wa Mataifa. Mbali na kulinda amani, askari hao tuliowatuma nje huchukua hatua za ziada na kufanya juu chini kuhakikisha kuwa maisha ya wananchi wa mataifa walikotumwa yanaboreka."

Rwanda ina takriban askari polisi wa kulinda amani 1,200 katika nchi za Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Haiti.

Kutokana na kushadidi machafuko, ukame na baa la njaa, mamia ya maelfu ya raia wa Sudan Kusini wameikimbia nchi na sasa wanaishi kama wakimbizi katika nchi jirani kama Sudan na Uganda.