Morocco yakubali kuunda serikali ya mseto kufumbua mkwamo wa kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26870-morocco_yakubali_kuunda_serikali_ya_mseto_kufumbua_mkwamo_wa_kisiasa
Waziri Mkuu mpya wa Morocco, Saadu Din al-Othmani amekubali kuunda serikali ya mseto itakayojumuisha vyama vingine vitano vya siasa , kwa shabaha ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa muda wa mrefu wa kisiasa nchini humo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Mar 26, 2017 02:01 UTC
  • Morocco yakubali kuunda serikali ya mseto kufumbua mkwamo wa kisiasa

Waziri Mkuu mpya wa Morocco, Saadu Din al-Othmani amekubali kuunda serikali ya mseto itakayojumuisha vyama vingine vitano vya siasa , kwa shabaha ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa muda wa mrefu wa kisiasa nchini humo.

Othmani ambaye aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wiki iliyopita na Mfalme Mohammed wa Sita wa nchi hiyo, anatokea Chama cha Uadilifu na Ustawi (PJD). Aliteuliwa kujaza nafasi ya Abdelilah Binkirane, ambaye alishindwa kuunda serikali ya muungano katika uongozi wake. 

Mfalme Mohammed wa Sita wa Morocco alimteua Binkirane Katibu Mkuu wa chama cha PJD kuwa Waziri Mkuu kufuatia ushindi wa chama hicho katika uchaguzi wa Bunge wa Oktoba 7 mwaka jana ambapo chama hicho kiliibuka na ushindi wa viti 125 bungeni.

Binkirane

Othmani amewaambia waandishi wa habari mjini Rabat kuwa, baraza lake jipya la mawaziri litajumuisha wadau wote wa kisiasa nchini humo, kwa lengo la kuimarisha uthabiti, mageuzi katika mfumo wa sheria, elimu, kawi na ustawi vijijini.

Mbali na chama cha PJD, vyama vingine vitakavyojumuishwa katika serikali hiyo ya mseto ni National Rally of Independents (RNI), Socialist Union of Popular Forces (USFP), Popular Movement (MP), Party of Progress and Socialism (PPS), na Constitutional Union (UC).