Watoaji misaada ya kibinadamu sita wauawa Sudan Kusini
Wahudumu sita wa asasi za kutoa misaada ya kibinadamu wameuawa katika mazingira ya kutatanisha nchini Sudan Kusini.
Eugene Owusu, afisa wa Shirika la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa OCHA amethibitisha kutokea mauaji hayo aliyoyataja kuwa ya kihaini na kuongeza kuwa, wafanyakazi hao waliuawa baada ya kutekwa nyara waliopokuwa wakisafiri kutoka mji mkuu Juba, wakilekea mji wa Pibor, mashariki mwa nchi.
Afisa huyo wa UN amebainisha kuwa, hii ni mara ya tatu kwa hujuma ya namna hii dhidi ya watoaji misaada ya kibinadamu kufanyika nchini humo mwezi huu wa Machi pekee.
Hivi karibuni, Elizabeth Ashamu Deng, mtafiti wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International nchini Sudan Kusini alisema kuwa, jeshi la serikali limechangia kuzidi kuharibika hali ya mambo nchini humo kwa kutowadhaminia usalama wafanyakazi wa asasi za kutoa misaada ya kibinadamu nchini humo.
Matamshi hayo yalitolewa siku chache baada ya Waziri wa Habari wa Sudan Kusini, Michael Makuei kutangaza kuwa, serikali itatoza kati ya dola 1000 hadi 10,000 za Marekani kwa raia wa kigeni wanaofanya kazi nchini humo kwa mwaka, kutoka dola 100, wakiwemo wafanyakazi wa asasi za kibinadamu.