Riek Machar: Natija ya kikao cha IGAD inakatisha tamaa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27094-riek_machar_natija_ya_kikao_cha_igad_inakatisha_tamaa
Kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini, Riek Machar ameonyesha kutofurahishwa na natija ya kikao cha Jumuiya ya Kieneo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 31, 2017 03:05 UTC
  • Riek Machar: Natija ya kikao cha IGAD inakatisha tamaa

Kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini, Riek Machar ameonyesha kutofurahishwa na natija ya kikao cha Jumuiya ya Kieneo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD).

Sambamba na kuashiria kuwa, matokeo ya kikao hicho yalikuwa yenye kuvunja moyo, Machar amesema kuwa, IGAD inashirikiana na serikali ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini katika kuwapuuza wapinzani wenye silaha nchini humo. Ameongeza kuwa, kikao cha Jumuiya ya Kieneo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) kimekiri kusambaratika makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka 2015 kwa ajili ya mzozo wa nchi hiyo.

Machar na Salva Kiir wakati walipokuwa pamoja katika uongozi

Sambamba na kusisitizia kwamba anaendelea kuheshimu makubaliano hayo baada ya kuangaliwa upya suala hilo na kutakiwa pande zote kuyaheshimu, kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini, Riek Machar amesema kuwa, ni jambo la kusikitisha kuiona IGAD inapuuza majukumu yake ya mchakato wa amani na kurejesha utulivu nchini Sudan Kusini. Kikao cha Jumuiya ya Kieneo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) kilifanyika wiki iliyopita mjini Nairobi, Kenya.

 Jumuiya ya Kieneo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD).

Washiriki wa kikao hicho mbali na kulaani makundi ya wabeba silaha nchini Sudan Kusini, waliyataka makundi hayo kuweka kando tofauti zao na kushiriki katika juhudi za kuitafutia ufumbuzi wa kisiasa migogoro ya nchi hiyio changa zaidi duniani. Mgogoro nchini Sudan Kusini ulizuka mwaka 2013, baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar kwamba anataka kumpindua.