Jeshi la Sudan Kusini lalaumiwa kwa kuteketeza vijiji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27128-jeshi_la_sudan_kusini_lalaumiwa_kwa_kuteketeza_vijiji
Vikosi vya jeshi la serikali ya Sudan Kusini viliteketeza maelfu ya nyumba mwishoni mwa mwaka jana wa 2016 wakati vita vya miaka mitatu vya wenyewe kwa wenyewe vilipokuwa vikiendelea nchini humo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 01, 2017 03:10 UTC
  • Jeshi la Sudan Kusini lalaumiwa kwa kuteketeza vijiji

Vikosi vya jeshi la serikali ya Sudan Kusini viliteketeza maelfu ya nyumba mwishoni mwa mwaka jana wa 2016 wakati vita vya miaka mitatu vya wenyewe kwa wenyewe vilipokuwa vikiendelea nchini humo.

Hayo yamesemwa na wasimamizi wa makubaliano ya amani yanayolegalega ya nchi hiyo na kuongeza kuwa, nyumba za vijiji vitatu kusini mwa mkoa wa Yei vilivyotembelewa na wachunguzi vimeteketezwa kwa moto na wakazi wake wameondolewa katika eneo hilo. Ripoti ya waangalizi wa makubaliano hayo inaeleza kuwa, nyumba nyingi zilichomwa moto kwa makusudi na vikosi vya jeshi la serikali.

Makubaliano ya amani yanayolegalega ya Sudan Kusini yalifikiwa mwaka 2015 kati ya serikali ya Juba na waasi.

Moja ya nyumba iliyochomwa moto katika mkoa wa Yei nchini Sudan Kusini 

Wakati huo huo maafisa wa serikali ya Sudan Kusini wamedai kuwa wapiganaji waasi na pia moto wa msituni ndio chanzo cha uharibifu huo. 

Jonathan Pedneault mtafiti katika shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch kuhusu Sudan Kusini amesema kuwa, wakati umefika kwa Rais Salva Kiir na makamanda wake kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kutokana na vitendo hivyo vya kikatili na kukiuka mara kadhaa sheria za kimataifa.

Katika upande mwingine ripoti nyingi ziliyotolewa na wasimamizi wa amani ya kimataifa zimeeleza kuwa vikosi vya jeshi la serikali ya Sudan Kusini na waasi nchini humo wamehusika kuwawinda na kuwateka nyara raia kusini mwa nchi hiyo.