Hatimaye serikali mpya ya mseto Morocco yaundwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27364-hatimaye_serikali_mpya_ya_mseto_morocco_yaundwa
Hatimaye serikali ya mseto ya Morocco imeundwa na viongozi kutoka vyama sita vyenye viti vingi bungeni ikiwa ni baada ya mkwamo wa kisiasa wa miezi sita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 06, 2017 03:19 UTC
  • Hatimaye serikali mpya ya mseto Morocco yaundwa

Hatimaye serikali ya mseto ya Morocco imeundwa na viongozi kutoka vyama sita vyenye viti vingi bungeni ikiwa ni baada ya mkwamo wa kisiasa wa miezi sita.

Serikali hiyo ya mseto inayoongozwa na Saad-Eddine El Othman, mbali na viongozi wa chama cha 'Uadilifu na Ustawi' ambacho kina viti vingi bungeni, kikiwa kinahodhi jumla ya viti 125 kati ya 395 vya bunge, viongozi wengine watatoka vyama vya National Rally of Independents (NRI), Socialist Union of Popular Forces (USFP), Popular Movement (MP), Party of Progress and Socialism (PPS) na Constitutional Union (UC).

Saad-Eddine El Othman alipoenda kuzungumza na Mfalme Mohammed VI

Tayari Mfalme Mohammed VI wa Morocco amekutana na kufanya mazungumzo na Saad-Eddine El Othman, Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa, Abdelilah Benkirane, waziri mkuu wa zamani wa Morocco wa chama cha 'Uadilifu na Ustawi' ambaye chama chake kilipata viti vingi katika uchaguzi uliopita, alishindwa kuunda serikali ya mseto baada ya miezi mitano ya juhudi kubwa za mazungumzo na viongozi wa vyama vya upinzani. Kutokana na hali hiyo, tarehe 17 Machi, Mfalme Mohammed VI wa nchi hiyo aliamua kumteua Saad-Eddine El Othman, mkuu wa baraza la kitaifa la chama hicho kuunda serikali. 

Vijana wa Morocco wanaolalamikia kukosa ajira

Inafaa kuashiria kuwa uundaji wa serikali nchini Morocco, unahitaji chama husika kupata viti 198 katika bunge la wawakilishi. Hii ni katika hali ambayo, ucheleweshaji katika kuundwa serikali mpya, uliibua migogoro ya kisiasa kati ya mirengo tofauti ya kisiasa nchini, katika hali ambayo taifa hilo bado linakabiliwa na migogoro mingine ya kiuchumi na kijamii.