Makumi ya wafungwa waachiliwa huru mashariki mwa Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i2743-makumi_ya_wafungwa_waachiliwa_huru_mashariki_mwa_kongo
Makumi ya wafungwa wameachiliwa huru mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 09, 2016 10:54 UTC
  • Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
    Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Makumi ya wafungwa wameachiliwa huru mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo.

Mkuu wa Mkoa wa Kivu Kusini, Marcellin Cishambo amesema kuwa, wafungwa 50 wa mkoa huo wamefutiwa adhabu zao kwa mujibu wa hukumu iliyotiwa saini na Waziri wa Mahakama wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mjini Kinshasa.

Marcellin Cishambo ameongeza kuwa, wafungwa hao 50 wamefaidika na msamaha uliotolewa na Rais Joseph Kabila mwaka 2014.

Watu hao walikamatwa kwa makosa ya kufanya uasi, jinai za kivita na makosa ya kisiasa.

Cishambo ameongeza kuwa, sehemu kubwa ya wafungwa hao walioachiliwa huru, ni wanamgambo wa makundi yenye silaha yaliyofanya mashambulizi katika maeneo ya Fizi na Uvira, huko Kivu Kusini.

Aidha amesema, wafungwa wengine 62 wataachiliwa huru kwa mujibu wa msamaha huo wa Rais Kabila, karibuni hivi.

Jela Kuu ya Bukavu huko Kivu Kusini ina uwezo wa kupokea watu 500 lakini hivi sasa kuna wafungwa 1,469 kwenye jela hiyo.