Wakimbizi wa njaa kutoka Somalia wamiminika Kenya
(last modified Tue, 11 Apr 2017 06:40:33 GMT )
Apr 11, 2017 06:40 UTC
  • Wakimbizi wa njaa kutoka Somalia wamiminika Kenya

Ukame ulioathiri sehemu mbalimbali Somalia umesababisha Wasomali wasiopungua 2,000 kuvuka mpaka na kuingia katika kambi ya Dadaab nchini Kenya katika miezi ya hivi karibuni. Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR.

Taarifa ya UNHCR inasema kuwa wakimbizi wengine wengi wako njiani kuelekea Dadaab,ili kutoroka ukame nchini Somalia.

Katika taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa inakadiriwa kuwa karibu wakimbizi 100 wapya waliowasili hivi karibuni ni miongoni mwa wakimbizi ambao walirudi Somalia kwa hiari kutoka kambi za wakimbizi za nchini Kenya ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuwarudisha kwao kwa hiari, wakimbizi wa Somalia.

Shirika hilo limesema, visa vya watu kukimbia makazi yao kutokana na ukame Somalia vimeongezeka maradufu.

Uhamiaji mkubwa wa watu walio na njaa na kiu katika kambi ya Dadaab utahatarisha au hata kurejesha nyuma hatua zilizopigwa miaka miwili nyuma za kuwarudisha kwa hiari wakimbizi nchini Somalia.

Kambi ya wakimbizi ya Daadab

Takriban raia wa Somalia 60,000 wamerudi nyumbani kutoka Dadaab tangu kuanzishwa mpango wa kurudi nyumbani kwa hiari mwezi Desemba 2014.

Umoja wa Mataifa unasema wakazi wa Dadaab 20,515 wamesaidiwa kurudi Somalia mwaka huu. Wengine 21,940 wamesajiliwa kwa ajili ya kurudi nyumbani kwa hiari.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaripoti kuwa kufikia tarehe 15 mwezi Machi mwaka huu idadi ya jumla ya wakimbizi katika kambi ya Dadaab ilikuwa ni 256,192.