Rwanda na Guinea Conakry kuimarisha uhusiano wao
Rwanda na Guinea Conakry zimesaini mikataba takriban saba ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga tofauti.
Makubaliano hayo yalisainiwa jana mwishoni mwa safari rasmi ya siku mbili ya Rais Paul Kagame wa Rwanda mjini Conakry. Rais Kagame amesema serikali ya Kigali itafanya juu chini kuona mikataba yote hiyo inatekelezwa tena kwa wakati uliopangwa. Mwenyeji wake Rais Alpha Conde kwa upande wake amepongeza juhudi za Rais Kagame za kutaka kuliona bara la Afrika linajitegemea katika kila nyuga na kukomesha utegemezi.
Miongoni mwa makubaliano yaliyosainiwa kati ya pande mbili hizo, ni kuondolewa vikwazo vya viza ili kuwepesisha uchukuzi na kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya pande mbili hizo.
Aidha serikali za Kigali na Conakry zimekubaliana kuwa zitaongeza safari zao za anga za moja kwa moja kwa shabaha ya kuboresha uchukuzi.