Watu wenye silaha waangamizwa katikati mwa Nigeria
Jeshi la polisi la Nigeria limetangaza habari ya kuuawa watu wawili katika jimbo la Niger la katikati mwa nchi hiyo.
Afisa mmoja wa ngazi za juu wa jeshi la polisi la Nigeria ametangaza habari hiyo na kusema kuwa jeshi hilo limepata idadi kubwa ya silaha za kila namna katika maficho ya magaidi hao.
Licha ya Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria kuahidi kumaliza makundi yenye silaha hasa Boko Haram wakati wa kampeni zake za uchaguzi, lakini serikali yake si tu haijayamaliza magenge hayo, bali mashambulizi ya makundi hayo hata yameongezeka.
Si hayo tu, lakini pia serikali ya Nigeria imeshindwa kuwakomboa wasichana waliotekwa nyara na Boko Haram huku kundi hilo la wakufurishaji likiendelea kuteka wasichana zaidi na kuwauza kama bidhaa.
Kundi la Boko Haram lilianzisha mashambulizi yake mwaka 2009 kaskazini mwa Nigeria na mwaka 2015 lilipanua wigo wa mashambulizi yake hadi katika nchi jirani za Niger, Chad na Cameroon.
Kundi hilo limeshaua zaidi ya watu 20 elfu katika nchi za Nigeria, Cameroon, Niger na Chad na kuwafanya wakimbizi watu milioni 2 hususan katika eneo la Ziwa Chad na kaskazini mashariki mwa Nigeria.