Waziri wa Ulinzi wa Marekani atembelea kituo cha kijeshi cha US, Djibouti
Waziri wa Ulinzi wa Marekani yuko nchini Djibouti katika kile kinachoonekana ni juhudi za Washington za kuimarisha na kupanua wigo wake wa kijeshi katika nchi za Afrika.
Shirika la habari la Reuters limeandika habari hiyo na kuongeza kuwa, James Mattis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani amekitembelea kituo cha kijeshi cha Washington, kusini mwa lango la Bahari Nyekundu, ambacho kimekuwa kikitumiwa kufanya mashambulizi ya Marekani dhidi ya Yemen na Somalia.
Kituo hicho cha kijeshi cha Marekani katika nchi hiyo ndogo ya Afrika chenye takriban wanajeshi 4000, kimekuwa kikitumiwa na US eti katika mashambulizi yake dhidi ya genge la kigaidi la al Qaeda katika Peninsula ya Kiarabu (AQAP).
Safari hii ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani nchini Djibouti ni sehemu ya safari yake ya kuzitembelea nchi kadhaa za Afrika na Mashariki ya Kati.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Alkhamisi iliyopita alifanya ziara ya siku moja nchini Misri na kuonana na Rais Abdul Fattah el Sisi na Sedki Sobhi, Waziri wa Ulinzi wa Misri. Pande mbili zilizungumzia ushirikiano wa nchi zao katika masuala ya kijeshi na kiusalama hususan hali ya mkoa wa Misri wa Sinai Kaskazini.
Mbali na kuzitembelea Saudi Arabia na Misri, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alielekea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel na kufanya mazungumzo na watawala wa Tel Aviv.