Maandamano makubwa ya kumtaka Rais Zuma ajiuzulu yafanyika Pretoria
Wananchi wa Afrika Kusini wameendelea kufanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi wakitaka kujiuzulu Rais wa nchi Jacob Zuma.
Jana mji wa Pretoria ulishuhudia maandamano makubwa ya kumshinikiza Rais Zuma ajiuzulu. Maandamano ya wananchi hao yaliyofanyika kwa mnasaba wa Siku ya Uhuru ambayo inasaidifiana na siku ya kufanyika uchaguzi wa kwanza huru nchini Afrika Kusini mwaka 1994 baada ya kuangushwa mfumo wa ubaguzi wa rangi nchini humo yalitoa wito wa kuachia ngazi Rais Zuma ambaye wanamtuhumu kwamba, ameshindwa kuiongoza nchi.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walisisitiza kwamba, Rais Zuma anapaswa kujiuzulu na kuondoka madarakani. Maandamano hayo yaliyowashirikisha watu wa matabaka mbalimbali wakiwemo wanaharakati wa asasi za kiraia yalikuwa ya aina yake.
Maandamano dhidi ya Rais Zuma yalishadidi zaidi baada ya mabadiliko aliyolifanyia Baraza la Mawaziri ambayo yamezusha mgogoro mpya kwa uongozi wake.
Uamuzi uliochukuliwa na Rais Zuma hivi karibuni wa kumtimua Waziri wa Fedha mwenye kuheshimika Pravin Gordhan umewakasirisha wapinzani na waungaji mkono wake na kudhoofisha nafasi yake mbali na kusababisha mpasuko ndani ya chama chake tawala cha ANC ambacho kinaiongoza Afrika Kusini tangu mwaka 1994 baada ya kuhitimishwa enzi za utawala wa wazungu wachache.
Aidha waandamanaji nchini Afrika Kusini wamekuwa wakidhihirisha hasira zao kutokana na kashfa mbalimbali za ubadhirifu, ukosefu wa ajira na kuzorota uchumi chini ya utawala wa Rais Zuma.