Mlipuko wa homa ya manjano kambini yaua watu 25 nchini Niger
(last modified Fri, 28 Apr 2017 07:49:21 GMT )
Apr 28, 2017 07:49 UTC
  • Mlipuko wa homa ya manjano kambini yaua watu 25 nchini Niger

Mlipuko wa homa ya manjano (Hepatitis E) umesababisha vifo vya makumi ya watu nchini Niger.

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limesema mlipuko huo umesababisha vifo vya watu 25 kufikia sasa katika kambi moja ya wakimbizi eneo la Diffa, kusini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Taarifa ya shirika hilo imesema kuwa: Kati ya Disemba mwaka jana na tarehe 23 mwezi huu wa Aprili, mbali na wanawake 25 wajawazito kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo, kesi 135 zimeripotiwa katika kambi hiyo.

Elmounzer Ag Jiddou, Mkuu wa Shirika la Madkatari Wasio na Mipaka nchini Niger amebainisha kuwa, mlipuko wa sasa wa Hepatitis E umesababishwa na ukosefu wa maji na mazingira machafu hususan vyoo.

Kambi ya wakimbizi ya Diffa nchini Niger

Siku chache zilizopita, Jumuiya ya Wasomaji Bingwa wa Qur'ani na taasisi nyingine zisizo za serikali za Niger ziliashiria uhaba wa suhula na hali mbaya inayowasibu wakimbizi katika miji ya Diffa na Boso huko kusini mashariki mwa Niger huku zikiwahimiza wananchi kushiriki katika jitihada za kuwasaidia wakimbizi hao. 

Eneo la Diffa ambalo liko katika mpaka wa Niger na Nigeria na lenye wakimbizi zaidi ya laki 3, limekuwa likitumiwa na wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika mashambulizi yake tangu mwaka 2015. 

Tags