UN yasema machafuko mapya Sudan Kusini yanaongeza mateso kwa raia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28444-un_yasema_machafuko_mapya_sudan_kusini_yanaongeza_mateso_kwa_raia
Umoja wa Mataifa umeeleza kusikitishwa na kuongezeka kwa machafuko na mateso kwa raia wa Sudan Kusini, kufuatia operesheni ya hivi karibuni ya jeshi la serikali ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 30, 2017 03:01 UTC
  • UN yasema machafuko mapya Sudan Kusini yanaongeza mateso kwa raia

Umoja wa Mataifa umeeleza kusikitishwa na kuongezeka kwa machafuko na mateso kwa raia wa Sudan Kusini, kufuatia operesheni ya hivi karibuni ya jeshi la serikali ya nchi hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika taarifa kupitia msemaji wake, Stephane Dujarric, ametoa wito kwa serikali ya Sudan Kusini na pande zingine hasimu kusitisha mapigano na kutimiza wajibu wao wa kulinda raia.

Aidha, Umoja wa Mataifa umezitaka pande hasimu kushirikiana nao na wahudumu wengine wa masuala ya kibinadamu ili kuhakikisha kuwa raia walioko hatarini magharibi mwa ukingo wa Mto Nile wanafikiwa salama.

Umoja wa Mataifa umesema kuongezeka upya kwa mapigano kunaonyesha kupuuzwa kwa ahadi zilizotolewa wakati wa mkutano wa IGAD wa Machi 25 2017, za kutekelezwa makubaliano ya usitishaji mapigano na kuwezesha ufikishaji misaada, na kukariri kuwa hapawezi kuwepo suluhu la kijeshi kwa mzozo wa Sudan Kusini.

Salva Kiir (kushoto) na Riek Machar

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.