Waziri auawa 'kimakosa' mjini Mogadishu, Somalia
Waziri wa Ujenzi na Ukarabati wa Somalia ameuawa kwa kupigwa risasi kimakosa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu.
Katika taarifa, serikali ya Somalia imesema imesikitishwa sana na mauaji ya Abbas Abdullahi Siraji mwenye umri wa miaka 31, ambaye alikuwa waziri mwenye umri mdogo zaidi nchini humo.
Siraji ambaye amekulia katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab nchini Kenya ameuawa kwa kupigwa risasi kimakosa na maafisa usalama, nje ya Ikulu ya Rais mjini Mogadishu.
Seneta wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, Ilyas Abdullahi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, Waziri huyo wa Ujenzi aliuawa baada ya walinzi wa Ikulu ya Rais kufyatulia risasi gari lake wakidhani ni la wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab.
Rais wa Somalia Mohammed Abdullahi Farmajo ambaye kwa sasa yuko katika ziara ya kikazi nchini Ethiopia, ametangaza kwamba atakatiza safari yake hiyo na kureje nyumbani kuomboleza kifo cha waziri huyo, huku akiahidi kwamba uchunguzi utafanyika kubaini kiina cha mauaji hayo.
Habari zaidi zinasema kuwa, vyombo vya usalama vinawazuilia walinzi wa Ikulu ya Rais waliohusika na mauaji hayo ya kutatanisha.