Baba wa mhusika wa shambulio la kigaidi la Manchester akamatwa nchini Libya
Baada ya kukamatwa ndugu wa kiume wa Salman Abedi, mhusika wa shambulio la kigaidi la mjini Manchester, Uingereza, kitengo cha kupambana na ugaidi nchini Libya kimetangaza kuwa kimemkamata pia baba wa mhusika huyo wa shambulio hilo.
Msemaji wa kitengo hicho Ahmed Bin Salem amesema Ramadhan Abedi, baba wa Salman Abedi, amekamatwa katika mji mkuu wa Libya, Tripoli kuhusiana na shambulio la kigaidi la siku ya Jumatatu usiku lililofanywa katika mji wa Manchester, Uingereza.
Hii ni katika hali ambayo kabla ya kutiwa nguvuni, baba huyo wa mhusika wa shambulio hilo alikanusha kuhusika mwanawe na hujuma hiyo akisema kuwa familia yao haiitakidi juu ya kuua watu wasio na hatia. Amesema Salman hakuwa na imani hizo na ana hakika hakufanya shambulio hilo la kigaidi na kwamba kuna mkono nyuma ya kadhia hiyo na kuwa maafisa usalama wa Uingereza wana kitu dhidi ya jamii ya Walibya walioko nchini humo hususan vijana.
Wakati huo huo Bin Salem ameeleza kuwa wana ushahidi kuwa Hashim Abedi, ndugu wa Salman Abedi alikuwa na uhusiano na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (IS) pamoja na kaka yake. Ameongeza kuwa wamekuwa wakifuatilia nyendo zake kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu na kwamba alikuwa na mawasiliano na kaka yake na alikuwa na taarifa kuhusu shambulio hilo.
Kwa mujibu wa msemaji wa kitengo cha kupambana na ugaidi nchini Libya Hashim, mwenye umri wa miaka 18 amekiri kuwa yeye na kaka yake Salman aliyekuwa na umri wa miaka 22 walikuwa wanachama wa Daesh.
Watu 22 waliuawa na wengine 59 walijeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea kwenye ukumbi wa muziki wa Manchester Arena, nchini Uingereza. Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh limetangaza kuhusika na shambulio hilo.../