Rais Kabila wa DRC atakiwa kuondoka madarakani
Kamanda wa zamani katika Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amemtaka Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo kuondoka madarakani.
Elie Kapend Kanyimbu jenerali wa zamani katika jeshi la DRC amesema Kabila anapaswa kuondoka madarakani Novemba 19 mwaka huu baada ya kumalizika duru ya pili ya urais.
Jenerali huyo amepinga pendekezo la Rais Kabila la kufanyika mazungumzo kuhusu uchaguzi ujao. Amesema kile kinachotakiwa ni kufanyika kongamano huru la kitaifa. Kanyimbu ni mwanzilishi wa kundi la wapiganaji wa AFDL ambalo lilimuondoa madarakani Mobutu Seseseko mwaka 1997 kwa uungaji mkono wa Uganda. Hivi sasa Kanyimbu ni mkuu wa chama cha upinzani cha FNLC.
Kwa miezi kadhaa sasa, jamii ya kimataifa imekuwa ikisisitizia umuhimu wa kufanyika uchaguzi mkuu katika tarehe iliyopangwa huko Kongo DR, huku waungaji mkono wa Rais Joseph Kabila wakitaka muda zaidi kwa ajili ya shughuli hiyo. Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, Rais Joseph Kabila haruhusiwi kugombea tena katika uchaguzi ujao.