Makamu wa Rais wa Afrika Kusini atuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa Kiir
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29644-makamu_wa_rais_wa_afrika_kusini_atuhumiwa_kupokea_rushwa_kutoka_kwa_kiir
Waasi nchini Sudan Kusini wamemtuhumu Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa kwamba amepokea rushwa kutoka kwa Rais Salva Kiir wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ili kuendelea kumzuilia kiongozi wao Riek Machar ambaye yuko nchini humo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
May 26, 2017 22:49 UTC
  • Makamu wa Rais wa Afrika Kusini atuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa Kiir

Waasi nchini Sudan Kusini wamemtuhumu Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa kwamba amepokea rushwa kutoka kwa Rais Salva Kiir wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ili kuendelea kumzuilia kiongozi wao Riek Machar ambaye yuko nchini humo.

Kanali Lam Paul Gabriel, Naibu Msemaji wa Kundi la waasi la SPLM LO ameliambia shirika la habari la Afrika Kusini la News24 kuwa, Ramaphosa amekuwa akipokea hongo kutoka kwa serikali ya Rais Kiir, ili ahakikishe Machar anaendelea 'kuzuiliwa' huko Afrika Kusini na harejei Juba.

Hata hivyo Ronnie Mamoepa, Msemaji wa Ofisi ya Makamu wa Rais wa Afrika Kusini amepuuzilia mbali madai hayo akisema kuwa hayana msingi na yanalenga kuivunjia heshima ofisi hiyo.

Rais Kiir (kushoto) na Machar

Mwishoni mwa mwezi uliopita, David Shearer, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini alisema aghalabu ya viongozi wa Jumuiya ya Kieneo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) pamoja na viongozi wa Afrika Kusini hawataki kabisa Machar aruhusiwe kurejea nchini Sudan Kusini wakisisitiza kuwa, yumkini kurejea kwake kukawasha moto zaidi wa mapigano na machafuko.

Machar alikimbilia Afrika Kusini mwishoni mwa mwaka jana, akidai kuwa wanajeshi watiifu kwa Rais Salva Kiir wanataka kumuua.