Umoja wa Afrika: Waafrika wahitimishe utegemezi wao kwa Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30000-umoja_wa_afrika_waafrika_wahitimishe_utegemezi_wao_kwa_magharibi
Rais wa Guinea ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kiduru wa Umoja wa Afrika amesema kuwa, bara la Afrika linapaswa kuhitimisha utegemezi wake kwa madola ya Magharibi.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jun 03, 2017 22:49 UTC
  • Umoja wa Afrika: Waafrika wahitimishe utegemezi wao kwa Magharibi

Rais wa Guinea ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kiduru wa Umoja wa Afrika amesema kuwa, bara la Afrika linapaswa kuhitimisha utegemezi wake kwa madola ya Magharibi.

Rais Alpha Conde amesisitiza kuwa, kuna haja na udharura sasa kwa mataifa ya Kiafrika kuachana na utegemezi wao kwa madola ya Magharibi na kujiainishia mustakabali wao yenyewe.

Mwenyekiti huyo wa Umoja wa Afrika AU amesema, haipasi kwa bara la Afrika kuendelea kuwa tegemezi kwa Wamagharibi bali nchi za bara hilo zinapaswa kujitegemea na kutoruhusu mataifa mengine kuingilia masuala ya ndani ya bara hilo.

Rais Alpha Conde amesema kuwa, bara la Afrika linapaswa kufikiria makubaliano ya biashara huru kwa ajili yake na kwa upande wa masuala ya kisiasa na kiuchumi, nchi za Afrika lazima zijiainishie zenyewe hatima na mustakabali wao na kutoruhusu wengine kufanya hilo.

Umasikini umekuwa ukiongezeka Afrika kutokana na utajiri uliopo barani humo kutosimamiwa vizuri

Aidha mwenyekiti huyo wa kiduru wa Umoja wa Afrika amebainisha kwamba, kwa sasa bara la Afrika limechukua hatua madhubuti za ustawi, kuongeza ukuaji wa uchumi na uzalishaji wa malighafi wa ndani, lakini kungali kuna njia ndefu mpaka kufikiwa malengo hayo.

Bara la Afrika lina utajiri mwingi wa maliasili, lakini wakazi wa bara hilo wamekuwa wakitaabika kwa umasikini kutokana na siasa mbovu za nchi nyingi za bara hilo na viongozi wa mataifa mengi ya Afrika kuwa vibaraka wa madola ya kikoloni ya Magharibi.