Makumi ya wahajiri wahofiwa kufa maji pwani ya Libya
Makumi ya wahajiri wanahofiwa kufa maji baada ya boti yao kuzama mashariki mwa Tripoli, mji mkuu wa Libya.
Issa al-Zaroog, msemaji wa Gadi ya Pwani ya Libya katika mji wa Garabulli amesema hadi kufikia sasa wamepata miili 8 ya wahajiri hao na kwamba yumkini boti hiyo ilikuwa imebeba wahajiri kati ya 100 na 110.
Naye Ayoub Qassem, msemaji wa Gadi ya Pwani ya Libya mjini Tripoli amesema mhajiri mmoja raia wa Bangladesh ameuawa na wengine wawili kujeruhiwa katika makabaliano ya risasi kati ya watu wanaofanya magendo ya wahajiri na maafisa wa Gadi ya Pwani ya Libya mjini Zawiya.
Wiki iliyopita, wahajiri saba wa Kiafrika walipoteza maisha baada ya kukosa hewa wakiwa ndani ya lori lenye jokofu kwa muda wa siku mbili katika pwani ya Libya.
Kwa mujibu wa Shirika la Wahajiri Duniani IOM, watu wanaofanya biashara haramu ya magendo ya wahajiri wanatengeneza faida ya dola bilioni 35 za Marekani kwa mwaka pasina na kujali namna wanavyohatarisha maisha ya maelfu ya wahajiri.
Mwaka uliopita pekee, wahajiri zaidi ya elfu tano aghlabau wakiwa raia wa nchi za Nigeria, Eritrea, Somalia, Sudan, Gambia, Senegal, Mali, Morocco na Tunisia Aghalabu walifariki dunia kwa kuzama katika bahari ya Medittaraenia wakiwa katika safari hizo hatari za kuelekea Ulaya, kwenda kutafuta kazi na maisha mazuri.