Marekani yadai kuua wanachama 8 wa al-Shabaab Somalia
Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika (AFRICOM) imedai kuwa shambulizi la anga la wanajeshi wake limefanikiwa kuangamiza wanachama wanane wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab kusini mwa Somalia.
Taarifa ya AFRICOM imesema hujuma hiyo ya anga ya US ya jana Jumapili ililenga ngome ya al-Shabaab karibu na mji wa Sakow, eneo la Juba ya Kati, yapata kilomita 300 kusini mwa mji mkuu, Mogadishu.
Rais Mohammed Abdullahi Farmajo wa Somalia amesema shambulizi hilo la anga la Marekani limelenga moja ya ngome muhimu za al-Shabaab na kwamba huenda litaathiri vibaya mustakabali wa genge hilo la kitakfiri.
Shambulizi hilo la anga la Marekani linaonekana kuwa la ulipizaji kisasi, kwani mwezi uliopita wa Mei, askari mmoja wa US aliuawa na wengine wawili kujeruhiwa katika makabiliano na wanamgambo wa al-Shabaab, katika eneo la Barii, yapata maili 40 magharibi mwa mji mkuu Mogadishu.
Itakumbukwa kuwa, Marekani iliviondoa vikosi vyake nchini Somalia mwaka 1993 kwa madhila, baada ya wanajeshi wake wasiopungua 18 kuuawa na kisha miili yao kuburutwa ardhini katika barabara za mji mkuu Mogadishu.