Niger yawaokoa wahajiri 92 waliotelekezwa kwenye jangwa la Sahara
Mamlaka za Niger zimewaokoa wahajiri 92 kutoka Afrika Magharibi waliokuwa wametelekezwa na wafanya magendo ya binadamu kwenye jangwa la Sahara wakijaribu kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Libya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na Giuseppe Loprete, mkuu wa timu ya Shirika la Kimataifa la Uhajiri (IOM) iliyotumwa nchini Niger, wahajiri hao ambao wengi wao ni raia wa Nigeria waliokolewa na timu ya shirika hilo ikishirikiana na askari wa Niger.
Niger ni kituo cha njiani kinachotumiwa na wahajiri wanaoelekea barani Ulaya, ambapo kwa mujibu wa baadhi ya wataalamu, wahajiri wengi zaidi wa Kiafrika wanafariki kwenye jangwa la Sahara kuliko wanaozama baharini.
Kwa mujibu wa Loprete, mmoja wa wahajiri hao alifariki muda mfupi baada ya kuwasili kwenye kituo cha IOM kilichoko kwenye mji wa Dirkou, kaskazini mashariki mwa Niger. Ameongeza kuwa wahajiri waliosalia watahamishiwa kwenye mji wa Agadez katikati mwa Niger kabla ya kusafirishwa na kurejeshwa nchi walikotoka.
Nchi za Ulaya zimeahidi kuipatia Niger makumi ya mamilioni ya dola kupambana na wafanya magendo ya binadamu; na kwa mujibu wa ripoti ya mwezi Aprili ya Shirika la Kimataifa la Uhajiri idadi ya wahajiri wanaovuka mpaka wa Niger kuelekea Libya imepungua tangu mwaka uliopita, zaidi ikiwa ni kutokana na hatua zilizochukuliwa na serikali ya Niamey za kupambana na magendo ya binadamu. Pamoja na hayo wahajiri zaidi ya 40 wamefariki dunia kwa kiu huko kaskazini mwa Niger mwezi huu huku timu za IOM zikiendelea kuwatafuta watu wengine 25 wanaoaminika kuwa wamepotea jangwani…/