Watu watano wauawa aktika hujuma ya kigaidi Mandera, Kenya
Watu watano wanaripotiwa kuuawa nchini Kenya katika mji wa El Wak kaunti ya Mandera eneo la kaskazini mashariki kufuatia hujuma ya kundi la kigaidi la al-Shabab.
Taarifa zinasema, mapema Ijumaa magaidi walishambulia eneo la makazi la mji wa mpakani wa El Wak na kuwaua raia watatu na maafisa wawili wa polisi. Aidha watu kadhaa wamejeruhiwa katika hujuma hiyo ya magaidi wa Kitakfiri wa al Shabab.
Akithibitisha kutokea hujuma hiyo, mkuu wa polisi katika eneo la Mandera Kusini Charles Chacha amesema watu walioshukiwa kuwa magaidi wa al-Shabab waliwashambulia polisi waliokuwa wakilinda Benki ya Equity mjini El Wak.
Duru zinadokeza kuwa magaidi kwanza waliwaua maafisa wa polisi katika mlango wa benki kabla ya kuwafyatulia raia risasi kiholela na baada ya hapo wakatoroka.
Katika wiki za hivi karibuni maafisa karibu 20 wa polisi ncini Kenya wameuawa katika barabara za eneo la kaskazini mashariki ambapo magaidi wamekuwa wakitega mabomu barabarani.
Kenya imekuwa ikikabiliwa na changamoto za usalama tokea mwaka 2011 wakati ilipotuma wanajeshi wake nchini Somalia kupambana na kundi la kigaidi la Al Shabab ambalo lilikuwa likishambulia maeneo ya kitalii nchini humo.