Libya yaitaka Saudi Arabia ieleze kwa nini imewatia mbaroni raia wake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31082-libya_yaitaka_saudi_arabia_ieleze_kwa_nini_imewatia_mbaroni_raia_wake
Serikali ya Libya imedhihirisha kukasirishwa kwake na kitendo cha Saudi Arabia cha kuwakamata raia wa nchi hiyo walipokuwa wanajiandaa kurejea nyumbani na kuitaka Riyadh itoe maelezo kuhusiana na sababu za kuwatia mbaroni raia hao wa Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 28, 2017 10:53 UTC
  • Jengo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya mjini Tripoli
    Jengo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya mjini Tripoli

Serikali ya Libya imedhihirisha kukasirishwa kwake na kitendo cha Saudi Arabia cha kuwakamata raia wa nchi hiyo walipokuwa wanajiandaa kurejea nyumbani na kuitaka Riyadh itoe maelezo kuhusiana na sababu za kuwatia mbaroni raia hao wa Libya.

Gazeti la al Yaum al Sabí la nchini Misri limenukuu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya iliyoitaka Saudia Arabia itoe maelezo ya kwa nini imewakamata raia wa Libya waliokwenda Saudia kufanya ibada ya Umra. Raia hao wa Libya wamekatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jiddah nchini Saudi Arabia wakati walipokuwa njiani kurejea nyumbani.

Baadhi ya vyombo vya habari vya Libya vilikuwa vimetangaza habari kuwa, raia wawili wa nchi hiyo walihusika katika kutekwa nyara wanadiplomasia watano wa Misri mwanzoni mwa mwaka 2014 huko Tripoli, mji mkuu wa Libya.

Moja ya maeneo ya kusubiria safari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jiddah, nchini Saudi Arabia

 

Wanadiplomasia hao wa Misri walitekwa nyara na kundi moja lenye silaha nchini Libya ambalo lilitaka kuachiliwa huru kiongozi wake aliyekuwa amekamatwa nchini Misri. Wanadiplomasia hao watano wa Misri waliachiliwa huru baadaye katika mkabala wa kuachiliwa huru kiongozi wa kundi hilo la Libya. 

Libya haijawahi kushuhudia utulivu tangu alipopinduliwa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi mwezi Oktoba 2011. Uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Libya ndiyo sababu ya kushindwa juhudi zote za kurejesha usalama katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.