Wanne wauawa 21 wajeruhiwa katika mapigano mapya karibu na Tripoli, Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31634-wanne_wauawa_21_wajeruhiwa_katika_mapigano_mapya_karibu_na_tripoli_libya
Wizara ya Afya ya Libya imetangaza kuwa, watu 25 wameuawa na kujeruhiwa katika mapigano yaliyotokea siku mbili zilizopita baina ya makundi hasimu mashariki mwa Tripoli, mji mkuu wa Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 11, 2017 10:15 UTC
  • Wanne wauawa 21 wajeruhiwa katika mapigano mapya karibu na Tripoli, Libya

Wizara ya Afya ya Libya imetangaza kuwa, watu 25 wameuawa na kujeruhiwa katika mapigano yaliyotokea siku mbili zilizopita baina ya makundi hasimu mashariki mwa Tripoli, mji mkuu wa Libya.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ufaransa, AFP, Wizara ya Afya ya Libya imetangaza kuwa, watu wanne wameuawa wakati wa mapigano baina ya kundi lililotangaza utiifu wake kwa serikali ya umoja wa kitaifa na makundi hasimu yenye mfungamano na serikali ya zamani ya nchi hiyo katika mji wa Qara Bolli‎ mashariki mwa Tripoli, mji mkuu wa Libya. Wawili kati ya watu waliouawa ni raia na mmoja ni mfanyakazi wa nchi ya kigeni.

Wapiganaji wa mkuu wa serikali ambayo ilikuwa haitambuliwi rasmi na ambaye aliamua kukaa pembeni baada ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya walikuwa wameweka kambi karibu na mji wa Qara Bolli tangu siku kadhaa nyuma.

Mapigano nchini Libya yamekuwa yakisababisha maafa mengi

 

Hadi leo hii Libya imeshindwa kuwa salama tangu Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO ulipoivamia nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kufanya mauaji makubwa pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu kwa madai ya kumpindua Kanali Muammar Gaddafi na baadaye kuitelekeza huku silaha za kila namna zikiwa zimezagaa mikononi mwa makundi tofauti mwaka 2011 .

Uingiliaji wa madola ya kigeni ya kieneo na kimataifa ndio unaolaumiwa kwa kushadidisha mgogoro nchini Libya kiasi kwamba juhudi zote za kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo zimekuwa zikikwama.