Human Rights Watch: Rwanda imewaua watu 37 kwa makosa madogo
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limesema katika ripoti yake kwamba, vikosi vya usalama nchini Rwanda vimewaua takriban watu 37 wanaoshukiwa kufanya makosa madogo madogo tangu mwezi Aprili mwaka jana.
Ripoti ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu inaeleza kuwa, wengi kati ya watu hao walituhumiwa kwa wizi wa mikungu ya ndizi, ng'ombe au hata pikipiki huku wengine wakishukiwa kuhusika na uingizaji wa mihadarati kama vile bangi kupitia mpaka wa Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo au makosa ya kutumia nyavu za kuvulia samaki zilizopigwa marufuku nchini humo.
Ripoti hiyo yenye kurasa 40 iliyopewa jina ''Wezi Wote Lazima Wauwawe'' na ambayo inaelezea mauaji hayo katika eneo la kaskazini mwa Rwanda imetoa maelezo ya kina ambayo yanaonyesha jinsi wanajeshi, polisi na vikosi vingine vya usalama nchini Rwanda vinavyo tekeleza mauaji hayo na mara nyingine vikiwa vinasaidiwa na raia.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, mauaji hayo yanachukuliwa kama njia mojawapo ya kueneza taharuki miongoni mwa raia kwa ajili ya kuwatisha wapinzani wa serikali huku nchi hiyo ikijiandaa na uchaguzi mkuu baadaye mwezi ujao.
Wakati huo huo, kampeni za uchaguzi wa Rais zinaanza rasmi leo nchini Rwanda huku Tume ya Uchaguzi ya nchiyo ikiwa imepasisha majina ya wagombea watatu tu wa kiti cha Urais baada yawagombea wengine kushindwa kutimiza masharti.