WFP: Dola 220 zinahitajika kwa ajili ya Zimbabwe
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limetangaza kuwa, linahitajia kiasi cha dola milioni 220 kwa ajili ya shughuli za misaada ya kibinadamu kwa nchi ya Zimbabwe inayokabiliwa na ukame.
Taarifa ya WFP imeeleza kuwa inahitaji kiasi hicho cha fedha kitakachotumika kwa ajili ya shughuli ya kupeleka misaada kwa wananchi wa Zimbabwe ambao wanataabika kutokana na ukame ulioikumba nchi hiyo.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani limesema fedha hizo ni bajeti ya shughuli hiyo hadi kufikia Machi mwaka 2017. Ripoti zinaeleza kuwa, idadi ya wananchi wa Zimbabwe wanaohitajia misaada ya kibinadamu imeongezeka kutoka milioni 3 na kufikia milioni nne.
Tangazo hili la WFP linatolewa mwezi mmoja tu baada ya Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kuutangaza ukame ulioikumba nchi hiyo kuwa ni janga la kitaifa. Inasemekana kuwa, vijiji vingi vya kusini mwa Zimbabwe vimepoteza mifugo ya ng'ombe na mazao kutokana na ukame mkubwa ulioikumba nchi hiyo.
Wakati huo huo, Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kushughulikia Watoto (UNICEF) umetahadharisha juu ya hali mbaya ya njaa nchini Zimbabwe na kutangaza kuwa, endapo hatua za lazima hazitachukuliwa, baa la njaa na utapiamlo vitavuka kiwango cha kushindwa kudhibitika. Mwezi uliopita serikali ya Harare iliomba msaada wa dola bilioni moja na milioni 600 kwa ajili ya kununua nafaka na bidhaa nyengine za chakula.