Abiria 14 wauawa na kujeruhiwa katika uvamizi Sudan Kusini
Abiria wanne wameuawa na wengine zaidi ya 10 wamejeruhiwa baada ya watu waliojizatiti kwa silaha kushambulia msafara wa mabasi nchini Sudan Kusini.
Polisi ya Sudan Kusini imesema, wavamizi hao waliushambulia msafara huo wa mabasi ya abiria jana Jumatano katika barabara kuu inayounganisha mji mkuu Juba na Nimule, katika mpaka wa nchi hiyo na Uganda, kusini mwa nchi.
Msemaji wa Polisi amethibitisha kutokea uvamizi huo na kuongeza kuwa vyombo vya usalama vinawasaka wahalifu waliotekeleza ukatili huo.
Hili ni shambulizi la pili dhidi ya magari ya abiria katika barabara hiyo kuu tangu mwezi Juni, ambapo watu 14 waliuawa na wengine 35 kujeruhiwa katika uvamizi wa kwanza.
Mauaji ya kiholela na vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.