Mbabe wa kivita wa DRC akabidhiwa kwa serikali ya Kinshasa
Mbabe wa kivita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambaye amekuwa akisakwa kwa udi na uvumba kutokana na jinai dhidi ya binadamu alizofanya amekabidhiwa na Umoja wa Mataifa kwa vyombo vya dola vya Kinshasa.
Bi. Fabienne Pompey, msemaji wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa Kongo DR MONUSCO ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, Ntabo Ntaberi Sheka amekabidhiwa kwa serikali ya Kinshasa, siku chache baada ya kujisalimisha kwao.
Sheka, ambaye anaandamwa na tuhuma za kufanya jinai dhidi ya binadamu ikiwemo kuwabaka wanawake kwa umati alijisalimisha kwa askari wa MONUSCO Julai 26, katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
Mbabe huyo wa kivita amekuwa akizuiliwa mjini Goma, makao makuu ya mkoa huo tangu baada ya kujisalimisha kwa kikosi hicho cha kusimamia amani cha UN.
Wanamgambo wanaoongozwa na mbabe huyo wa kivita ndani ya kundi la waasi wa Mai-Mai Sheka ni tawi la makundi yanayobeba silaha huko mashariki mwa Kongo ambayo mara mara yamekuwa yakituhumiwa na Umoja wa Mataifa na makundi ya kutetea haki za binadamu kuwa yanatumia vitendo vya ubakaji kama silaha yao ya kivita.
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limeitaka serikali ya Kongo DR kumdhaminia usalama mbabe huyo wa kivita ambaye alikuwa katika orodha nyeusi ya Umoja wa Mataifa, mbali na kuzuiwa mali zake na kuwekewa vikwazo vya kusafiri popote duniani.