Al-Shabaab yawakata vichwa watu 3 kaunti ya Lamu, Kenya
Kwa akali watu watatu wameuawa kwa kukatwa vichwa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabab katika kaunti ya Lamu, pwani ya Kenya.
Kamishna wa kaunti hiyo, Gilbert Kitiyo amethibitisha kutokea mauaji hayo yaliyofanyika katika kijiji cha Maleli, eneobunge la Witu, Lamu Magharibi. Kadhalika magaidi hao wameteketeza kwa moto nyumba kadhaa katika eneo hilo.
Hata hivyo kamishna huyo hajatoa maelezo zaidi kuhusu tukio hilo, ingawaje anasema maafisa usalama wametumwa katika eneo hilo kudhibiti mambo.
Hii si mara ya kwanza kwa genge hilo la Kiwahabi kushambulia kaunti ya Lamu na kutorokea katika msitu wa Boni ulioko katika kaunti hiyo.
Mapema mwezi uliopita wa Julai, wanachama wengine wa al-Shabab waliwauwa kwa kuwakata vichwa watu 9 katika shambulizi lililofanyika katika kijiji kimoja cha kaunti hiyo ya Lamu, siku chache baada ya wanamgambo wa kundi hilo la kigaidi kuua polisi watatu katika kijiji jirani cha Pandanguo na baadaye wakaua wanafunzi wanne na polisi wanne katika kijiji cha Kiunga, kaunti hiyo ya Lamu.
Aidha mwezi Mei mwaka huu, maafisa saba wa polisi ya utawala waliuawa baada ya gari lao kukanyaga bomu lililotegwa kando ya barabara katika kaunti ya Lamu, kusini mashariki mwa Kenya.