Polisi ya Rwanda yaanza kumchunguza mkosoaji wa Rais Paul Kagame
Polisi ya Rwanda imesema kwamba inamchunguza Diane Shima Rwigara, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Rais Paul Kagame wa nchi hiyo kwa tuhuma za kukwepa kulipa ushuru na kughushi.
Rwigara alizuiliwa kushiriki katika uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni nchini humo, suala ambalo limekosolewa na nchi za Magharibi.
Hata hivyo Jeshi la Polisi la Rwanda ambalo limefanya msako katika nyumba ya familia ya Diane Shima Rwigara, limekadhibisha uvumi unaosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba mpinzani huyo wa Kagame ametiwa nguvuni.
Rwigara mwenye umri wa miaka 35 amekuwa akimshutumu Rais Paul Kagame wa Rwanda kuwa anakandamiza na kubinya upinzani na kwamba chama chake cha Rwandan Patriotic Front (RPF) kinahodhi madaraka yote ya nchi.
Tume ya Uchaguzi ya Rwanda ilimzuia Diane Shima Rwigara kuchuana na Rais Kagame katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais wa mwezi uliopita wa Agosti kwa hoja kwamba, hakuweza kukusanya saini zinazohitajika za waungaji mkono wake na kwamba baadhi ya majina aliyoyatuma kwa tume hiyo yalikuwa ya watu waliofariki dunia. Rwigara amekanusha amadai hayo.
Rais Paul Kagame wa Rwanda anasifiwa kimataifa kwa kurejesha amani nchini Rwanda na kustawisha uchumi wa nchi hiyo haraka baada ya kukomesha mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994. Hata hivyo kiongozi huyo analaumiwa na jumuiya za kutetea haki za binadamu kwamba, anabana uhuru wa vyombo vinavyojitegemea vya habari na kukandamiza wapinzani wake.