Serikali ya Somalia yakiri kuua raia katika operesheni ya pamoja na Marekani
Serikali ya Somalia hatimaye imekiri kwamba raia 10 wa Kisomali waliuawa eti kimakosa katika operesheni ya pamoja iliyofanywa na jeshi la nchi hiyo na askari wa Marekani Ijumaa iliyopita.
Akiongea kwa niaba ya serikali hii leo katika shughuli ya kuwazika wahanga hao, Mohamed Ahmed Abtidon, Mbunge wa Somalia amesema ni kweli raia hao waliuawa katika operesheni ya pamoja na jeshi la Marekani katika kijiji cha Bariire, ingawaje anasisitiza kuwa waliuawa kwa bahati mbaya.
Mbunge huyo ameongeza kuwa, serikali inafanya mazungumzo na familia za wahanga wa hujuma hiyo kuhusu suala la kulipwa fidia.
Mkuu wa Baraza la Wazee wa kijiji cha Bariire amesema walifikia muafaka na serikali jana jioni na kuruhusu kuzikwa watu hao, ikizingatiwa kuwa, awali, familia za wahanga wa shambulizi hilo zilikataa kuzika maiti za wapendwa wao wakiwemo watoto watatu mpaka serikali ikubali kubeba dhima ya mauaji yao yaliyofanywa katika shambulio lililotekelezwa kwa msaada wa jeshi la Marekani.
Watu hao 10 waliuliwa kwa kupigwa risasi wakati jeshi la Somalia likisaidiwa na askari wa Marekani lilipofanya operesheni ya shambulio katika kijiji cha Bariire kilichoko kilomita zipatazo 50 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu Ijumaa iliyopita.
Awali jeshi la Somalia lilitangaza kuwa watu wote waliouliwa katika shambulio hilo la Ijumaa walikuwa wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab linalopambana nalo kwa msaada wa Marekani na vikosi vya Umoja wa Afrika AMISOM.