Mafuriko yameua watu 50 nchini Niger na kuacha maelfu bila makazi
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, kwa akali watu 50 wamefariki dunia nchini Niger kufuatia maafa ya mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa imebainisha kwamba, kwa uchache watu 50 wamefariki dunia nchini Niger katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita kutokana na mvua kali zilizoambatana na mafuriko na kwamba, watu laki moja na elfu ishirini wamebakia bila makazi baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko hayo.
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imetangaza kuwa, mji mkuu Niamey ndio ulioathirika zaidi na mafuriko hayo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, miji mingine iliyokumbwa na mafuriko nchini Niger ni ya Dossa ulioko kusini, Tillaberi wa magharibi, Maradi na Zinder iliyopo katikati mwa nchi hiyo.
Taarifa ya Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa, nyumba karibu elfu kumi na shule zimeharibiwa na mafuriko katika mji mkuu Niamey.
Baadhi ya mashirika ya utoaji misaada ya kibinadamu yametangaza kuwa, hali ya kibinadamu katika baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na mafuriko ni mbaya.
Mwaka jana pia Niger ilikumbwa na mafuriko ambapo zaidi ya watu 50 walipoteza maisha.
Mafuriko hayo yanatokea huku nchi hiyo ikikabiliwa na changamoto mbalimbali likiwemo suala la uhaba wa chakula na ukosefu wa usalama katika baadhi ya maeneo kutokana na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram.