Duru ya pili uchaguzi wa rais Niger bila mpinzani
Duru ya pili ya kiti cha rais nchini Niger imefanyika leo huku kukiwa na hali tete ya usalama na wapinzani wakisusia zoezi hilo na mgombea wa pili akiwa anapata matibabu Ufaransa.
Rais wa sasa Mahamadou Issoufou anatazamiwa kupata ushindi katika uchaguzi huu wa leo ambao matokeo yake yanatazamiwa kutangazwa katika kipindi cha siku tano zijazo.
Katika duru ya kwanza ya uchaguzi mwezi Februari asilimia 67.46 ya wananchi wa nchi hiyo walishiriki ambapo Issoufou aliibuka wa kwanza kwa kupata zaidi ya asilimia 48 ya kura. Hama Amadou, Waziri Mkuu wa zamani wa Niger ambaye kwa sasa yuko jela alijipatia asilimia 17 ya kura na kushika nafasi ya pili. Siku ya Jumatano Amadou alikimbizwa hospitalini Ufaransa kufuatia ombi lake binafsi. Jina lake liko katika makaratasi ya kura lakini wapinzani wamesema wanasusia uchaguzi.
Tarehe pili Machi viongozi wa kambi ya upinzani waliitaka serikali ya Niger imuachie huru mwanasiasa huyo ili aweze kufanya kampeni zake kwa uhuru na kushindana na mgombea wa chama tawala. Kambi ya upinzani pia imewasilisha rasmi mashtaka katika Mahakama Kuu ya Niger ikidai kulifanyika wizi wa kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais. Madai hayo yanapingwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Niger ambayo imesema uchaguzi ulifanyika kwa uhuru na uadilifu.
Karibu watu milioni saba na nusu wametimiza masharti ya kupiga kura katika uchaguzi wa leo.