Mahakama ya Juu Kenya yatoa ufafanuzi wa kubatilisha uchaguzi wa urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34621-mahakama_ya_juu_kenya_yatoa_ufafanuzi_wa_kubatilisha_uchaguzi_wa_urais
Mahakama ya Juu nchini Kenya imesema haijuti kuchukua uamuzi wa kubatilisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8 mwaka huu, huku ikiilaumu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC kwa kuendesha zoezi hilo kinyume cha sheria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 20, 2017 09:47 UTC
  • Mahakama ya Juu Kenya yatoa ufafanuzi wa kubatilisha uchaguzi wa urais

Mahakama ya Juu nchini Kenya imesema haijuti kuchukua uamuzi wa kubatilisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8 mwaka huu, huku ikiilaumu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC kwa kuendesha zoezi hilo kinyume cha sheria.

Majaji watatu kati ya wanne waliopiga kura ya kubatilishwa matokeo hayo wameilaumu IEBC kwa kuanza kupeperusha matokeo ya urais kabla ya kuyafanyia uhakiki wakisisitiza kuwa katiba, sheria na kanuni za uchaguzi zilikiukwa pakubwa.

Wamesisitiza kuwa, kasoro zilizokuwepo zilikuwa nyingi na zilizoratibiwa kwa makusudi kiasi cha kuathiri matokeo na kwamba suala la kutokuwepo uwazi katika upeperushaji wa matokeo pia linatia shaka.

Kadhalika majaji hao wa Mahakama Kuu ya Kenya wamekosoa hatua ya IEBC ya kutotii agizo la mahakama la kufungua sava za tarakilishi zake ili zifanyiwe uchunguzi na wataalamu wa teknolojia wa muungano wa upinzani NASA.

Rais Kenyatta (kushoto) na kinara wa upinzani Raila Odinga

Hapo jana polisi nchini Kenya walilazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa chama cha Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta ambao waliandamana nje ya Mahakama ya Juu wakipinga uamuzi wa kubatilisha uchaguzi huo wa rais.

Muungano wa upinzani wa NASA umesisitiza kuwa hautashiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Oktoba 17 iwapo masharti uliyoyatoa hayatatekelezwa. Kutokota mgogoro ndani ya uongozi wa IEBC na kauli ya kampuni ya teknolojia ya OT-Morpho ya Ufaransa iliyopewa zabuni ya kuwasilisha mfumo wa kupeperusha matangazo ya urais kuwa yumkini hautakuwa tayari kufikia tarehe iliyotajwa; ni miongoni mwa mambo yanayoashiria kuwa uchaguzi huo wa marudio yumkini yasifanyike Oktoba 17.