19 wauawa katika mapigano kwenye mpaka wa Sudan na Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34729-19_wauawa_katika_mapigano_kwenye_mpaka_wa_sudan_na_libya
Habari kutoka nchini Sudan zinasema kuwa, watu 19 wameuawa katika mapigano yaliyotokea kwenye maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Libya.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Sep 23, 2017 01:04 UTC
  • 19 wauawa katika mapigano kwenye mpaka wa Sudan na Libya

Habari kutoka nchini Sudan zinasema kuwa, watu 19 wameuawa katika mapigano yaliyotokea kwenye maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Libya.

Hassan Muhammad Abdullah, mmoja wa makamanda wa askari wa radiamali ya haraka wa Sudan katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Libya alisema jana usiku kuwa, mapigano baina ya wanajeshi wa nchi hiyo na wafanya magendo ya binadamu yamepelekea watu 19 kuuawa ambao ni wanajeshi wawili wa Sudan na wafanya magendo 17.

Magendo ya binadamu nchini Libya

 

Amesema, askari wa Sudan wamezuia pia kuingia nchini Libya kinyume cha sheria watu wengine 41 wenye uraia wa nchi mbalimbali na wamewatia mbaroni viongozi saba wa makundi ya magendo ya binadamu.

Kamanda huyo wa kijeshi wa Sudan ameongeza kuwa, askari wa Sudan wamekamata magari saba ambayo yalikuwa yamewekwa silaha tayari kwa mashambulizi.

Libya haijawahi kushuhudia utulivu hata mara moja tangu muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi NATO ulipoingia kijeshi nchini humo mwaka 2011 na kumpindua kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.

Magenge ya magendo ya binadamu yanatumia ukosefu wa utulivu Libya kufanya magendo

 

Ukosefu wa amani nchini Libya umesababisha matatizo pia kwa nchi jirani kama vile Sudan kwani Libya hivi sasa imekuwa kituo kikuu cha magendo yakiwemo ya binadamu huku magenge mbalimbali ya uhalifu yakitumia fursa hiyo kuendesha uhalifu wao kwa uhuru nchini Libya.