Libya yajibu mapigo, kuwazuia Wamarekani kuingia nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34969-libya_yajibu_mapigo_kuwazuia_wamarekani_kuingia_nchini_humo
Serikali ya Libya yenye makao makuu yake mashariki mwa nchi, imesema haitaruhusu raia wa Marekani kuingia katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, ikiwa ni radiamali kwa hatua ya Washington kuwapiga marufuku Walibya kuingia Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 28, 2017 10:58 UTC
  • Libya yajibu mapigo, kuwazuia Wamarekani kuingia nchini humo

Serikali ya Libya yenye makao makuu yake mashariki mwa nchi, imesema haitaruhusu raia wa Marekani kuingia katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, ikiwa ni radiamali kwa hatua ya Washington kuwapiga marufuku Walibya kuingia Marekani.

Taarifa ya serikali hiyo inayoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar imesema hatua hiyo ya Marekani kuzuia raia wa Libya kusafiri nchini humo ni hatari na ambayo itazidi kuvuruga mambo badala ya kujenga.

Imesema marufuku hiyo itakayoanza kutekelezwa rasmi Oktoba 18 haijatolewa kwa lengo la kupambana na vitendo vya ugaidi bali ina ajenda fiche.

Hivi karibuni, Rais Donald Trump aliziongeza Korea Kaskazini, Chad na Venezuela katika orodha ya nchi ambazo raia wao hawaruhusiwi kufanya safari nchini Marekani. 

Bendera ya Libya

Nchi nyingine ni Iran, Syria, Libya, Somalia na Yemen, huku Sudan iliyokuwa katika orodha ya awali ikiondolewa katika orodha mpya.

Libya ilidhani kwamba nayo ingeondolewa katika orodha hiyo mpya ya Trump, iliyotangazwa Jumatatu iliyopita.