Marais wa Kenya na Uganda wanakutana jijini Nairobi kujadili bomba la Mafuta
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni wanakutana leo jijini Nairobi kwa shabaha ya kujadili ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kati ya nchi hizo mbili.
Mkutano huo unafanyika siku chache tu baada ya Uganda na Tanzania kuafikiana kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta kutoka bandari ya Tanga nchini Tanzania hadi nchini Uganda. Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Kenya ni miongoni mwa miradi iliyo kwenye mpango mkubwa wa miradi ya miundo mbinu ya kanda ya kaskazini (NCIP). Makampuni yanayozalisha mafuta nchini Uganda, kampuni ya Tullow kutoka Ireland, kampuni ya Ufaransa ya Total na kampuni ya CNOC kutoka Uchina, zimealikwa kuhudhuria katika mkutano huo wa Nairobi baina ya Rais Uhuru Kenyatta na mgeni wake Yoweri Museveni wa Uganda.
Bomba hilo la mafuta lilikusudiwa kutumiwa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima hadi bandari ya Lamu, kupitia eneo lenye mafuta Kenya la Lokichar.
Viongozi hao wawili walikutana nchini Uganda Agosti mwaka jana na kuafikiana kwamba ujenzi wa bomba hilo ulifaa kuharakishwa.
Mpango huo unaonekana kushindana na mpango wa Uganda wa kushirikiana na Tanzania kujenga bomba la kusafirisha mafuta.
Tanzania inataka ujenzi huo uanze haraka na wiki iliyopita Makamu wa Rais wa kampuni ya Total Afrika Mashariki Bw Javier Rielo alimwambia Rais wa Tanzania John Magufuli, kuwa kampuni hiyo itaanza ujenzi huo haraka iwezekanavyo, kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zipo.