Rwanda yamshtaki mkosoaji wa Rais kwa kuchochea uasi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35221-rwanda_yamshtaki_mkosoaji_wa_rais_kwa_kuchochea_uasi
Msemaji wa Mwendesha Mashtaka wa serikali ya Rwanda amesema leo kuwa, mamlaka husika za Rwanda zimemfungulia mashtaka mkosoaji wa Rais Paul Kagame kwa kosa la kuchochea uasi na kughushi baada ya kuzuiwa kuchuana na hasimu wake Kagame katika uchaguzi wa rais wa mwezi Agosti mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 04, 2017 12:43 UTC
  • Rwanda yamshtaki mkosoaji wa Rais kwa kuchochea uasi

Msemaji wa Mwendesha Mashtaka wa serikali ya Rwanda amesema leo kuwa, mamlaka husika za Rwanda zimemfungulia mashtaka mkosoaji wa Rais Paul Kagame kwa kosa la kuchochea uasi na kughushi baada ya kuzuiwa kuchuana na hasimu wake Kagame katika uchaguzi wa rais wa mwezi Agosti mwaka huu.

Diane Shima Rwigara aliye na umri wa miaka 35 ambaye ni mhasibu kitaaluma amekuwa akimtuhumu Rais Kagame kwa kuwabinya wapinzani na kukikosoa chama tawala cha RPF kwa kuweko madarakani tangu kiliposhika hatamu za uongozi na kuhitimisha mauaji ya kimbari nchini humo mwaka 1994. Kagame alishinda uchaguzi huo wa rais kwa kupata asilimia 98.8 ya kura.

Rais Paul Kagame wa Rwanda  

Mama yake Diane Rwigara, Bi Adeline na dada yake aliyetajwa kwa jina la Anne pia wameshtaki kwa uchochezi, ubaguzi na udini. Hayo yameelezwa na Mwendesha Mashtaka Faustin Nkusi. Wanawake hao watatu wamekuwa korokoroni kwa wiki zipatazo mbili. Tarehe 30 mwezi Agosti watuhumiwa hao walichukuliwa nyumbani kwao Kigali  kwa madai ya kudaiwa kukwepa kulipa kodi zinazoihusu kampuni ya tumbaku inayomilikiwa na familia hiyo. Hata hivyo tuhuma hii ya kukwepa kulipa kodi haijajumuishwa katika tuhuma zilizosomwa jana dhidi yao.