Mpinzani wa Rais Kagame, Diane Rwigara afikishwa mahakamani Rwanda
Mwanasiasa wa upinzani nchini Rwanda na mkosoaji mashuhuri wa Rais Paul Kagame wa nchi hiyo Diane Rwigara, mamake na dadake leo walifikishwa mahakamani mjini Kigali kwa mara ya kwanza zikiwa zimepita wiki mbili baada ya kushikiliwa na polisi.
Diane Shima Rwigara anatuhumiwa kughushi na kufanya udanganyifu katika fomu alizojaza kwa ajili ya kugombea urais Agosti mwaka huu akitaka kuchuama na Rais Kagame. Hata hivyo baadaye aliondolewa katika kinyanganyiro hicho baada ya kushindwa kutimiza masharti.
Tume ya uchaguzi ya Rwanda ilisema kwamba alifanya ulaghai katika kutafuta saini za wafuasi wake ili kutimiza matakwa ya tume hiyo.
Tangu ulipoanza mchakato huo wa kutaka kuingia ikulu,Diane Rwigara amejitokeza kama mpinzani na mkosoaji mkuu wa chama tawala RPF.
Duru za karibu na mahakama mjini Kigali zinasema kuwa, watatu hao wameshitakiwa kwa kuchochea uasi nchini Rwanda, mashtaka wanayokanusha wakisema yana misingi ya kisiasa.
Diane Shima Rwigara aliye na umri wa miaka 35 ambaye ni mhasibu kitaaluma amekuwa akimtuhumu Rais Kagame kwa kuwabinya wapinzani na kukikosoa chama tawala cha RPF kwa kuweko madarakani tangu kiliposhika hatamu za uongozi na kuhitimisha mauaji ya kimbari nchini humo mwaka 1994.
Tarehe 30 mwezi Agosti watuhumiwa hao walichukuliwa nyumbani kwao Kigali kwa madai ya kukwepa kulipa kodi zinazoihusu kampuni ya tumbaku inayomilikiwa na familia hiyo. Hata hivyo tuhuma hii ya kukwepa kulipa kodi haijajumuishwa katika tuhuma wanazokabiliwa nazo hivi sasa.
Baadhi ya duru zinaikosoa serikali ya Rais Kagame na kuitaja kesi hiyo kwamba, ina matamshi ya kisiasa.