Waasi washambulia kituo cha askari wa Umoja wa Mataifa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35471-waasi_washambulia_kituo_cha_askari_wa_umoja_wa_mataifa_drc
Duru za kuaminika huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimesema kuwa, waasi wa Uganda wameshambulia kituo cha askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa mashariki mwa Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 10, 2017 04:42 UTC
  • Waasi washambulia kituo cha askari wa Umoja wa Mataifa DRC

Duru za kuaminika huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimesema kuwa, waasi wa Uganda wameshambulia kituo cha askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa mashariki mwa Kongo.

Habari kutoka Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimesema kuwa, askari wawili wa Umoja wa Mataifa wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulio hilo lililofanywa na waasi wa Uganda wanaojiita kwa jina la Kikosi cha Pamoja cha Demokrasia. Shambulio hilo limefanyika katika kambi ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Askari wa Umoja wa Mataifa MONUSCO Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, karibu raia 20 wameuawa katika shambulio hilo la waasi wa Uganda, mashariki mwa Kongo.

Tangu mwaka 1994 hadi hivi sasa, waasi wa Uganda wamekuwa wakifanya mashambulizi katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mamia ya watu wameshauawa hususan katika eneo la Beni la mkoa wa Kivu Kaskazini.

Machafuko katika maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanaendelea kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Kushindwa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na askari wa kofia buluu wa Umoja wa Mataifa kulinda usalama wa raia na kuyamaliza magenge ya waasi kumepelekea kuongezeka ukosefu wa amani na utulivu katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika.