UN yatahadharisha kuhusu mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati
Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ametahadharisha kuhusu uwezekano wa kushadidi zaidi mgogoro wa nchi hiyo.
Najat Rochdi amekiambia kikao kinachofanyika katika mji mkuu wa Cameroon, Younde kwamba, mgogoro wa ndani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati unapanuka zaidi baada ya kujitokeza ukatili na mapigano mapya kati ya makundi ya waasi kwa ajili ya kudhibiti maliasili hususan migodi ya almasi na dhahabu.
Rochdi amesema katika kikao hicho kinachofanyika kwa shabaha ya kukusanya misaada ya kifedha ya kukabiliana na athari mbaya za mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwa, machafuko yanashadidi zaidi nchini humo kila uchao na askari wa jeshi la nchi hiyo na wale wa kimataifa hawana uwezo wa kuboresha hali hiyo.
Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ameongea kuwa, zaidi ya nusu ya jamii ya watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanahitajia misaada ya kibinadamu na kwamba hali ya wakimbizi laki sita miongoni mwao inatia wasiwasi mkubwa.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013 na kiongozi mpya wa nchi hiyo, Faustin-Archange Touadera ameshindwa kurejesha amani na utulivu nchini humo.